“Itakuwa Fainali Ya Aina Yake”, Kerr, Djuma Waizungumzia Gor Mahia VS Simba - Sports Kitaa | PressTZ - Your Number 1 Source of Aggregated Online Content

 

“Itakuwa Fainali Ya Aina Yake”, Kerr, Djuma Waizungumzia Gor Mahia VS Simba

NAKURU, Kenya – Homa inazidi kupanda kuelekea mchezo wa fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup itakayopigwa hapo kesho kwenye dimba la Afraha mjini hapa kati ya mabingwa watetezi Gor Mahia na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara, Simba SC.

Kuelekea mchezo huo wa kukata na shoka utakaopigwa kuanzia majira ya saa tisa kamili alasiri, makocha wa timu zote mbili wameongea na vyombo vya habari kuelezea mitazamo yao kuhusiana na mechi hiyo.

Umaliziaji butuAkizungumza kwa upande wa Simba SC, Kocha Masoud Djuma alianza kwa kueleza kinaga ubaga cha timu yake kutofunga goli lolote kwenye mashindano haya ndani ya dakika 90 licha ya kuweza kufika fainali.

“Jinsi tutacheza kiufundi itabaki kuwa siri ya Simba lakini hatujafungwa goli na hatujafunga lakini naamini kwasababu wachezaji wa mbele ni wapya kwenye timu yetu na mfumo tunaocheza hawajauzoea.

“Hawajaingia kwenye mfumo sawa sawa lakini tunajaribu kuona jinsi gani wataingia kwenye mfumo haraka ili waweze kutusaidia kwenye mechi ya fainali”, alifafanua.

Hata hivyo Djuma alielezea jinsi gani timu yake itaathirika kwa kumkosa kiungo Haruna Niyonzima ambaye atakuwa akitumikia adhabu ya kadi mbili za njano alizozipata kwenye michezo iliyopita.

“Kuhusu Niyonzima, tupo na wachezaji 17 ukimtoa yeye na wakati mwalimu akipanga kikosi huku akijua fulani hayupo basi lazima abadilishe mambo kulingana na hali halisi na mimi nitafanya hivyo kesho”, alisema.

Nafasi ya Mashabiki.
Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerry ataingia kwenye fainali hii kucheza dhidi ya timu ambayo aliwahi kuifundisha miaka miwili iliyopita huku pia akisisitiza umuhimu wa mashabiki kuelekea kwenye mechi hiyo.

“Simba ni timu nzuri lakini itakuwa mechi ngumu na tunatakiwa kwenda na akili sawa lakini tuna faida ya kuwa na mashabiki wetu kama ambavyo Simba wangekuwa nyumbani wangepata nafasi nzuri kwasababu ya mashabiki wao na ninaweza kusema kuwa nina bahati ya kufanya kazi na timu zote mbili kwasababu zina mashabiki wenye mapenzi ya dhati.


Mashabiki wa Gor Mahia wakishangilia ushindi wa timu yao dhidi ya Singida United kwenye mechi ya nusu fainali. (Picha – SPN)

“Ni nafasi nzuri kwasababu sijawahi kuwaaga mashabiki wa Simba vizuri. Uzuri wa mpira ukipata heshima kutoka kwa wachezaji uliowahi kuwafundisha na mapokezi wanayokupa pindi unapopata nafasi ya kuwaona tena ni kitu kinachokuonesha jinsi gani umefanya kazi nzuri kama kocha”, alizungumza Kerry kwa hisia kali.

Hali kadhalika Masoud Djuma kwa upande wake amesema kucheza ugenini hakuwapi shida kwani ni kama watakuwa nyumbani tu.

“Hata kama tunacheza ugenini na hata kama mashabiki wa Gor Mahia watakuwa wengi sisi tutawaona hao mashabiki wao kama wamevaa jezi nyekundu za Simba na kama wakizomea sisi tutaona kama wanatushangilia kwahiyo sisi tutacheza kwa kujituma zaidi”, alihitimisha Djuma.

Safari ya Everton
Licha ya kucheza dhidi ya Everton mwaka jana, lakini bado Kerr ameonesha nia ya kuitaka nafasi hiyo kwa mara nyingine tena endapo kama watafanikiwa kushinda mechi ya fainali dhidi ya Simba.

“Kila timu inayokuja kwenye haya mashindano inataka kucheza kwenye fainali ambayo tupo na itakuwa mechi ngumu kwa sababu ya zawadi.

Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerry (kulia) pamoja na nahodha wa timu hiyo, Harun Shakava (kulia) wakiongea na wana habari kuelekea mechi yao ya fainali dhidi ya Simba SC. Picha/SPN

“Sio kila mtu atapata nafasi ya kwenda Uingereza. Ndio, tumecheza na Everton mwaka jana lakini tunataka kucheza nao tena na itakuwa ni nafasi nzuri kwa wachezaji wangu kuwa sehemu ya mechi ya maandalizi ya Everton kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

“Ni ndoto ya kila mchezaji kucheza kwenye jiji kubwa kama Liverpool, kwenye uwanja mkongwe kama Goodison Park dhidi ya timu yenye mashabiki wengi na historia kubwa kama Everton”, alisisitiza Kerry.

Shauku ya kwenda Uingereza haitakuwa kwa wachezaji tu kama ambavyo anasema Kerr bali hata kocha wa Simba, Masoud Djuma nae anaonekana kuitolea macho haswa.

“Kila mtu anataka kwenda Uingereza. Mimi binafsi nilienda nikiwa mdogo lakini niliishia Uwanja wa ndege kwahiyo sikupata nafasi ya kuingia mjini.

“Kuishia uwanja wa ndege siwezi kusema ndio nimefika Uingereza kwahiyo mimi pamoja na wachezaji wangu tunaichukulia nafasi hii kwa uzito wa hali ya juu lakini kwanza inabidi tuhakikishe tunaifunga Gor Mahia kwenye fainali”, alizungumza Djuma huku akiachia cheko.

Penati au Dakika 90?
Mwisho wa siku ni bingwa mmoja tu atapatikana iwe ndani ya dakika 90 au kwa mikwaju ya penati huku kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerry akitamani zaidi kumaliza shughuli ndani ya dakika 90 akiamini Simba watampa shida kama akifika nao hatua ya penati.

“Simba wameonesha uwezo mzuri kwenye mikwaju ya penati na najua inaweza kumsumbua golikipa wangu lakini ukishakuwa kwenye hatua ya fainali unahitaji kujiamini kwahiyo tunaamini tutamaliza mechi ndani ya dakika 90 ingawa mpira ni mchezo wa ajabu”, alisema Kerr.

Simba wamefika fainali baada ya kuzitoa timu za Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz kwa mikwaju ya penati baada ya sare ya 0-0 huku Gor Mahia wenyewe wakijizolea umaarufu kwa kumaliza shughuli ndani ya dakika 90 dhidi ya JKU (3-0) na Singida United (2-0)


Source: Sports KitaaRead More