JESHI LA POLISI PWANI LATOA ZAWADI ZA IDDI NA KUFUTURISHA WATOTO YATIMA KITUO CHA KULELEA WATOTO FADHILA MISUGUSUGU - Issa Michuzi | PressTZ - Your Number 1 Source of Aggregated Online Content

 

JESHI LA POLISI PWANI LATOA ZAWADI ZA IDDI NA KUFUTURISHA WATOTO YATIMA KITUO CHA KULELEA WATOTO FADHILA MISUGUSUGU

Na Mwamvua Mwinyi, PwaniKAMANDA wa polisi mkoani Pwani (ACP) Jonathan Shanna,amewataka wananchi wenye uwezo kimaisha kutumia sehemu ya vipato vyao kuwezesha watoto yatima badala ya kuwaachia jukumu hilo wamiliki wa vituo vya kulelea watoto hao pekee.Aliyasema hayo wakati jeshi hilo lilipojumuika katika Iftar ya pamoja na watoto yatima wa kituo cha Fadhila kilichopo eneo la Misugusugu Kibaha na kutoa zawadi ya sikukuu ya Eid el Fitr kwa watoto hao.Alisema hakuna mtoto aliyependa kuwa yatima katika maisha yake ila kwa kuwa kifo ni wajibu kwa binadamu watoto hao wamejikuta wakiondokewa na wazazi wao."Hakuna ajuaye kesho yake ,watoto hawa hawakujua kama wangekuwa katika maisha haya ,ila ni kutokana na wazazi wao kufariki kwa sababu mbalimbali na kujikuta wamekuwa yatima" alisema kamanda Shanna.
Kamanda Shanna alieleza moja ya sababu zinazosababisha vifo ni ajali za barabarani ambazo nyingi hutokana na uzembe wa madereva kuyapita magari mengi bila ya kuchukua tahadhari na mwendo kasi.Alisema ajali hizo husababisha vifo na majeruhi hali inayopelekea tegemezi kupoteza wazazi wao jambo ambalo linaweza kudhibitiwa iwapo kila mmoja atashirikiana na jeshi la polisi kwenye kuwafichua madereva wasiotii sheria za usalama barabarani kwa makusudi. Kamanda huyo alisema, jeshi hilo kama chombo cha wananchi, limesukumwa kwa kurudisha fadhila za ushirikiano wanaopatiwa na wananchi katika kutanzua na kuzuia uhalifu ."Tumeguswa kwa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kuja kufturisha watoto yatima ambao ni sehemu ya jamii yenye kuhitaji kutazamwa kwa karibu ili nao kujiona hawajatengwa na jamii inayowazunguka" alisisitiza. Aidha kamanda Shanna alitoa mbuzi, mafuta ya kula, sabuni za kufulia, unga, sukari na Mchele.Kwa upande wake katibu wa kituo hicho Suraiya Mohammed, alilishukuru jeshi la polisi mkoa wa Pwani kwa kufuturu nao pamoja na zawadi ya sikukuu ya Eid el Fitr kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho .
Aliomba wasiishie katika mwezi mtukufu pekee bali wapatapo nafasi wafanye hivyo na kwa kipindi kingine kwani uhitaji wa msaada katika kuendesha kituo hicho kilicho na idadi ya watoto zaidi ya 150 ni mkubwa. Kamanda wa polisi mkoani Pwani (ACP) Jonathan Shanna  akiongea machache kabla ya kukabidhi vitu mbalimbali kwa ajili ya sikukuu ya Idd el Fitr kwa katibu wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Fadhila kilichopo Misugusugu Kibaha, Suraiya Mohammed, wakati jeshi hilo lilipokwenda kufturu pamoja na watoto 150 wanaolelewa kwenye kituo hicho.Kamanda wa polisi mkoani Pwani (ACP) Jonathan Shanna akikabidhi vitu mbalimbali kwa ajili ya sikukuu ya Idd el Fitr kwa katibu wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Fadhila kilichopo Misugusugu Kibaha, Suraiya Mohammed, wakati jeshi hilo lilipokwenda kufturu pamoja na watoto 150 wanaolelewa kwenye kituo hicho.


Source: Issa MichuziRead More