Kwanini Conte sio kocha mbovu, ila ni meneja mbovu - Shaffih Dauda | PressTZ - Your Number 1 Source of Aggregated Online Content

 

Kwanini Conte sio kocha mbovu, ila ni meneja mbovu

Antonio Conte amefukuzwa rasmi Chelsea. Kushindwa kucheza Uefa msimu ujao ndio kitendaliwi ambacho Roman hakuwa tayari kukitegua.


Conte hakuwa na msimu mzuri sana. Ndio amemfunga Mourinho fainali ya FA lakini kwa Roman ni kama umemtusi ikiwa anajua mwakani Chelsea hawapandi ndege kwenda nje ya taifa la England kushindana.Swali linakuje hapa, je ni nini hasa sababu kubwa ya Conte kutimuliwa? unahisi ni msimu mbovu? Ingekuwa hivyo angeshatimuliwa kitambo! Sasa kwanini wamesubiri hadi sasa bila kumfukuza? walikuwa wanajadiliana nini?


Kwangu mimi siamini sana kama amefukuzwa eti kisa sio kocha mzuri! La hasha!


Tatizo ni bodi.


Bodi ya Chelsea imekaa vikao mara kadhaa vikiongozwa na Mwenyekiti wao bwana Bruce Buck. Nyuma ya Buck kuna watendaji kama watatu: Marina Granovskaia, Guy Laurence, Eugene Tenenbaum.Mwezi machi mwaka huu Chelsea walikuwa nyuma ya City alama 22 wakiwa nafasi ya 5. Conte alipoulizwa mbona amekwama alisema ” Sina hela, unatarajia nifanyeje? kwanza mimi sio kocha kilaza, unapokuwa na kocha kama mimi unapaswa ujue upo na mtu wa aina gani”


Ukitazama kwa undani hili neno sina hela ni kama alitupa kombora kwa uongozi wa Chelsea.Nyuma ya watendaji wakuu kuna mjumbe: David Barnard, pamoja na wawakilishi wa raisi wa maisha wa chelsea Lord Attenborough CBE 1923-2014, ambao ni Sir Peter Harrison, Joe Hemani, Anthony Reeves na Alan Spence. Hawa wote walitoka na kauli moja kwamba Conte sio meneja mzuri.


Maamuzi ya usajili yalitoka juu. Na yalikuwa tofauti na zamani kipindi Roman ananunua wachezaji peke yake. Wakati huu wajumbe wa bodi lazima wakubali.Unadhani yale ni maamuzi ya kumtimua Conte ni ya Roman Abramovic mwenyewe? Hapana! Kuna watu nyuma yake. Kuna wawekezaji ambao wameifanya Chelsea izidi kuimarika.

Roman anavyozidi kuzeeka busara nazo zinamjia. Ndio maana imefika wasaa anavumilia bodi ifanye maamuzi. Lakini tukumbuke kitu. Wakati Chelsea inafanya usajili mwaka jana na mwaka huu Conte alilalamika kwamba bodi inafanya maamuzi bila kumshirikisha. Je ulitegemea bodi hii hii imwache salama Conte?Chelsea pia ina wawekezaji sio Roman pekee, wapo watu wengine ambao wana mamlaka na anawasikiliza. Mtu kama Bruce Michael Buck huyu ni msimamizi wa Globalworth Real Estate Investments Limited na ni mwenyekiti wa bodi, yupo Alan Shaw, Ron Gourlay, Eugene Alexander Tenenbaum msimizi EVRAZ. Wote hawa walivurugana na Conte. Tena huyo Tenenbaum alianza kuitumikia Chelsea siku ya kwanza tu Chelsea imenunuliwa na Roman mwaka 2003. Unadhani huyu mtu akimshauri Roman atakataa? Roman tunayemjua sisi alikuwa hawezi kumvumilia kocha ambaye timu inayumba. Hajawahi kuwa na roho hiyo kabisa. Tatizo lilianza kwa Conte mwenyewe kwa kuishtumu bodi kwenye mkutano wa waandishi wa habari.Mbali na hayo binafsi naona ametimuliwa kwa sababu sio meneja mzuri pia.


Kwa mawazo yangu mimi, mtu anaweza kuwa kocha mzuri lakini asiwe meneja mzuri. Kwa mfano, Conte alikuja na mfumo wa 4 1 4 1. Akapigwa vitatu na Arsenal. Michezo iliyofuata akabadilisha na kutumia 3 5 2. Huu ulikuwa sio mfumo pendwa sana EPL wala haaukuwa na mafanikio sana. Tokea alipoanza kutumia mfumo huo Chelsea lishinda michezo 13 mfululizo na usisahau kipigo cha haja alichotoa kwa Mourinho cha Mikwaju minne. Kuna mtu atakaa kwamba Chelsea walisumbua na mfumo ule? Wangapi walikuja nao wakayumba? Van Gaal si alikuja kwa mbwembwe mara abebe makaunta buku? Yuko wapi? Brendan Rodgers nae yu hali gani?Chelsea walijiweka mahali salama kwa kuweka mazingira kwamba wao walikuwa timu ngumu zaidi kuifunga. Conte alifanikiwa kushinda michezo 30 kwa msimu na kuweka rekodi mpya darajani. Walicheza kitimu na walikamilika kila idara. Alibadilisha upepo mzima. Alifufua hata wale waliopoteza dira (Victor Moses).


Msimu uliopita alikwama wapi?


Ukiachana na sakata lake la kutibuana na bodi, msimu uliopita Conte alifeli namna ya kumeneji wachezaji wake. Hajafeli ufundishaji wake uwanjani.Kitendo cha kuingia kwenye migogoro na wachezaji muhimu ndiko kuliko mfelisha. Alishindwa kumeneji tabia za wachezaji na hata hisia zake mwenyewe. Kama hili sakata lake na bodi. Pia tulisikia namna alivyomtumia Diego Costa ujumbe ambao haukuwa wa kistaarabu kabisa. Ugomvi wake na wasaidizi, maneno ya kashfa kwa mashabiki, kushindiwa kujizuia hasa hasa mihemko yake ya vita ya maneno na Mourinho, ugomvi wake na David Luiz yote haya yalimjengea sifa mbaya.TAKWIMU ZA JUMLA


Amecheza michezo– 76

Ameshinda– 51

Sare– 10

Amepoteza– 15

Wastani wa Ushindi — 67.1%

Magoli — 147

Yakufungwa — 71.


Makombe: EPL 2017, EFA 2018.


Conte ni mkorofi haswa. Kwanza mimi nilidhani Conte ataandika barua ya kuondoka klabuni hapo yeye mwenyewe.Nakumbuka niliwahi kuandika makala inayohusu tabia za Conte na Maisha yake ndani ya Chelsea.


Bonyeza hapa kufungua makala hiyo


Makala na Privaldinho (Instagram)


Source: Shaffih DaudaRead More