LUKUVI AOKOA MABILIONI MPAKA WA TANZANIA NA KENYA - Issa Michuzi | PressTZ - Your Number 1 Source of Aggregated Online Content

 

LUKUVI AOKOA MABILIONI MPAKA WA TANZANIA NA KENYA

Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameokoa takriban shilingi bilioni 16 za upimaji wa mpaka kati ya Tanzania na Kenya mara baada kuanza kazi ya upimaji wa mpaka huo wenye urefu wa jumla za kilomita 760 za nchi kavu.
Akiongea jana wakati akikagua kazi ya uwekaji wa alama mpya za mipaka iliyowekwa katika wilaya ya Tarime mkoani Mara Waziri Lukuvi amesema hapo awali wataalamu wa upimaji wa mpaka huo waliandaa makisio ya bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 22 ambapo mara baada kuanza kwa zoezi hilo amegundua kwamba zoezi hilo litagharimu shilingi bilioni 6 hadi kumalizika kwake.
“tulipanga kutumia shilingi bilioni 22 zilizokuwa katika makaratasi ambapo katika uhalisia tangu kuanza kwa kazi hii ya uwekaji alama mpya za mipaka tumegundua ya kwamba serikali inaweza kutumia shilingi bilioni 6 tu ambazo zitamaliza kazi hii ya uwekaji wa alama za mipaka kati ya Tanzania na Kenya” amesema Lukuvi.
Aidha, Waziri Lukuvi amewapongeza watendaji wa Idara ya Upimaji na Ramani iliyopo Wizara ya Ardhi inayoongozwa na Dkt. James Mtamakaya kwa kazi nzuri ya kizalendo iliyopelekea kuokoa fedha za serikali kwa kushirikiana na wataalam wa Mkoa na Halmashauri.
Ameongeza kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya mipango ya fedha katika makaratasi na uhalisia wa kazi katika eneo husika, mara baada ya kuanza kazi katika maeneo husika ya uwekaji wa alama mpya za mpaka kati ya Tanzania na Kenya imebainika kiuhalisia kazi hiyo haitatumia kiasi kikubwa cha fedha kama ilivyokisiwa hapo awali.
Waziri Lukuvi amefanya ziara hiyo ya ukaguzi wa mpaka wa Tanzania na Kenya ambapo juzi amekagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la mpaka lililopo wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na jana amekagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la mpaka lililopo wilaya ya Tarime Mkoani Mara.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akikagua alama za mpaka wa Tanzania na Kenya.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA


Source: Issa MichuziRead More