MAKAMU WA RAIS AWASILI MKOANI SONGWE KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU TANO - Issa Michuzi | PressTZ - Your Number 1 Source of Aggregated Online Content

 

MAKAMU WA RAIS AWASILI MKOANI SONGWE KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU TANO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili mkoani Songwe tayari kwa ziara ya siku tano.

Makamu wa Rais amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Lt. Mstaafu Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makala pamoja na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga na Viongozi wengine wa Chama na Serikali.

Akiwa mkoani Songwe, Makamu wa Rais atakagua na kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo ambapo atatembelea Wilaya Tatu za Mkoa huo ambazo ni Mbozi, Momba na Ileje. Makamu wa Rais ataanzia ziara yake katika Wilaya ya Mbozi ambapo miongoni mwa shughuli atakazofanya ni pamoja na kukagua na kufungua kituo cha Afya Nanyala, kusalimia wananchi katika eneo la mradi la Nanyala, kuweka jiwe la Msingi katika Mradi wa maji Iyula na kufanya Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Iyula.

Makamu wa Rais pia atatembelea Wilaya ya Momba ambapo atakagua na kuzindua kituo cha Afya Tunduma, atakagua shughuli za vikundi vya wajasiriamali Tunduma na kufanya mkutano wa hadhara kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Momba.

Vilevile, Makamu wa Rais atatembelea Wilaya ya Ileje ambapo atapokea taarifa ya shughuli za uhifadhi wa mazingira na upandaji miti na kukagua shughuli za uhifadhi na shamba la miti la Wakala wa Misitu Tanzania lilopo Katengele na baadae kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Isoko ambapo atapata fursa ya kuzungumza na wananchi wa Ileje.

Mhe. Makamu wa Rais atahitimisha ziara yake Mkoani Songwe tarehe 25, Julai 2018.

Imetolewa na;
Ofisi ya Makamu wa Rais
Julai 21, 2018
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili mkoani Songwe na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa Songwe Mhe. Lt. Mstaafu Chiku Galawa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makala na Viongozi wengine wa Chama na Serikali katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia baadhi ya viongozi wa Chama cha CCM,mara baada ya kuwasili mkoani Songwe na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa Songwe Mhe. Lt. Mstaafu Chiku Galawa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makala na Viongozi wengine wa Chama na Serikali katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).


   


Source: Issa MichuziRead More