MO AKUBALI KUNUNUA ASILIMIA 49 YA HISA ZA KLABU YA SIMBA - Issa Michuzi | PressTZ - Your Number 1 Source of Aggregated Online Content

 

MO AKUBALI KUNUNUA ASILIMIA 49 YA HISA ZA KLABU YA SIMBA

Na , Humphrey Shao, Globu ya Jamii 
MFANYABIASHARA maarufu nchini Mohammed Dewji 'Mo' amekubali kununua asilimia 49 za hisa za Klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali katika mchakato wa mabadiliko ya klabu hiyo kuwa kampuni.
Hayo yamethibitishwa leo jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Klabu ya Simba ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka huu Haji Manara wakati anazungumza na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya klabu yao.
Pia Manara amesema wanachama wa Simba SC wajitokeze kwa wingi katika mkutano wa mabadiliko ya Katiba utakaofanyika Mei 20 mwaka huu katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini.
"Mkutano huo ulioitishwa na Kaimu Mwenyekiti, Salim Abdallah ‘Try Again’ utaanza Saa 3:00 asubuhi na tayari wanachama wamekwishasomewa ajenda kwa mujibu wa Ibara ya 22 ya klabu hiyo, kufungu cha nne,"amesema Manara.
Ameongeza mkutano huo unakuja baada ya kufanyika mkutano wa Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mfanyabiashara Mo Dewji kuwa Mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji wa Simba SC.Mo pekee aliweka dau la Sh.bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
Wanachama 1,320 walihudhuria mkutano uliofanyika Desemba na walitoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia na hosteli ya kisasa ya wachezaji.


Source: Issa MichuziRead More