WINGA WA ZAMANI WA NIGERIA EMMANUEL AMUNIKE NDIYE KOCHA MPYA WA TAIFA STARS - Bin Zubery | PressTZ - Your Number 1 Source of Aggregated Online Content

 

WINGA WA ZAMANI WA NIGERIA EMMANUEL AMUNIKE NDIYE KOCHA MPYA WA TAIFA STARS

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amemtambulisha winga wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Karia amemtambulisha Amunike mwenye umri wa miaka 47 katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam jioni hii baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Emmanuel Amunike (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam

Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
Mayanga aliiongoza Taifa Stars kwa mara ya mwisho Machi 27, mwaka huu ikishinda 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Siku hiyo, mabao ya Tanzania yalifungwa na Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani yanayoipa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Taifa Stars inakuwa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.
Zaidi ya hapo, Amunike mwenye umri wa miaka 47 amefundisha kalbu za Al Hazm kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 aliporejea nyumbani kufunisha Ocean Boys.
Alipoachana na U17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda wengi, Taifa Stars.  
Kisoka, Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya.
Alianza na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I'Cons ya Korea Kusini kabla ya mwaka 2003 kwenda kumalizia soka yake Busan I'Cons alikocheza hadi 2004 akahamia Al-Wehdat ya Jordan.


Source: Bin ZuberyRead More